Maadhimisho siku ya ushirika kufanyika julai 3 na 4 Dodoma
26 June 2026, 15:51

Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa kila mwaka Jumamosi ya kwanza ya mwezi Julai. Mwaka huu, maadhimisho hayo yatafanyika Jijini Dodoma katika Ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete kuanzia Julai 3 hadi 4. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Na Elizabeth Tanzania.
Wananchi wa Jijini Dodoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yatakayofanyika kwa siku mbili, Julai 3 na 4, ili kupata uelewa wa kina kuhusu umuhimu na mchango wa vyama vya ushirika katika maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, amesema maadhimisho hayo yatawakutanisha wanachama wa vyama vya ushirika kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao watashiriki uzoefu wao na kueleza faida wanazozipata kupitia vyama hivyo.
Amesema vyama vya ushirika vimeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa wanachama wake kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi. Amefafanua kuwa, kwa mfano, wanachama wa vyama vya akiba na mikopo hupata fursa ya kukopa na kuongeza mitaji yao, jambo linalowawezesha kupanua shughuli zao za uzalishaji na biashara.
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo, “Ushirika kwa Dunia Yenye Amani,” Chitinka amesema lengo ni kuhimiza misingi ya haki, upendo na ushirikiano kama nguzo muhimu za maendeleo endelevu kupitia vyama vya ushirika.