Wakulima watakiwa kutumia mfumo wa anwani za makazi
6 August 2026, 17:38

Mhandisi Turuka ametoa wito kwa wananchi wote wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili kupata elimu na kujisajili au kusasisha taarifa zao katika Mfumo wa Anwani za Makazi, hatua ambayo itawawezesha kunufaika zaidi na huduma za kidijitali zinazotolewa nchini.
Na Anwary Shanani.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewahimiza wananchi, hususan wakulima, kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi kwa kuwa unarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma nchini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Anwani za Makazi kutoka Wizara hiyo, Mhandisi Edith Turuka, wakati wa Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nanenane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo vya Dkt. John Samuel Malecela.
Mhandisi Turuka amesema wizara inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa, ikiwemo usalama wa mtandao, mifumo ya kidijitali ya Serikali na Mfumo wa Anwani za Makazi, ambao umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuunganisha watoa huduma na wananchi.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Mhandisi Turuka amesema mfumo huo unawasaidia wakulima kupokea bidhaa na huduma kwa urahisi zaidi, kwa kuwa anwani sahihi huwezesha pembejeo za kilimo, vifaa na huduma nyingine kufikishwa moja kwa moja katika maeneo husika.