Bei mpya ya kodi ya vibanda vya biashara mamlaka ya mji mdogo Kongwa yatajwa
24 July 2026, 16:44

Sambamba na hayo wafanyabiashara wamekubaliana na Serikali kusaini mikataba mipya na kulipa kodi mpya iliyoongezwa kwa maendeleo ya Wilaya ya Kongwa.
Na Mariam Kasawa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka s Mayeka amekutana na wamiliki wa vibanda pamoja na wafanyabiashara wanaofanya biashara zao katika maeneo ya kituo cha mabasi Kongwa, Posta na sokoni kujadili kuhusu umiliki halali wa vibanda vya biashara na mabadiliko ya bei mpya ya kodi katika maeneo hayo.
Akiongea wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa elimu Kongwa Mhe. Mayeka amefafanua kuwa kulingana na sheria ya ardhi namba 4 na 5 mmiliki halali wa vibanda vya biashara vilivyopo maeneo hayo ni Serikali yaani Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na kwamba wafanyabiashara walioviendeleza (wamiliki) wanahesabika kuwa wapangaji.

Aidha Mayeka Ameongeza kuwa kutokana na Tozo za awali za vibanda hivyo kuwa ndogo (TSh. 5,000) na kupitwa na wakati kuanzia sasa Tozo itakuwa shilingi 20,000 kwa mwezi kwa banda moja kwa mchanganuo wa 70% ambayo ni sawa na shilingi 14,000 ambayo itaenda Halmashauri ili kuchangia mapato ya ndani na 30% sawa na shilingi 6,000 itaenda kwa mmiliki wa kibanda ili kufidia ujenzi wa kibanda chake.
Kwa upande wao wafanyabiashara waliofika katika mkutano huo wamesema kuwa awali kulikuwa na sintofahamu ya umiliki halali wa mabanda hayo kutokana na kutokupewa elimu juu ya umiliki wa ardhi.