Dodoma FM

Kampuni ya mixx by yas kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya tiba asili nchini

5 August 2026, 16:43

Meneja Mauzo wa Mixx by Yas akikabidhi kadi kwa wanachama zitakazo rahisisha mawasilianao katika shughuli zao. Picha na Anwary Shabani.

Kwa kutoa msaada huo wa mawasiliano, Mixx by Yas inaendelea kuonesha dhamira yake ya kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi wa shughuli za maendeleo katika jamii.

Na Anwar shabani.                                               

Kampuni ya Mixx by Yas imeendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha sekta ya tiba asili nchini kwa kukabidhi kadi maalumu za mawasiliano kwa wanachama wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili Tanzania (TAMESO-T) tawi la Kibaigwa, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, hatua inayolenga kurahisisha mawasiliano na kuboresha utendaji wa chama.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mauzo wa Mixx by Yas anayesimamia wilaya za Kongwa na Mpwapwa, Christian Lenadi, amesema kampuni hiyo imeamua kushirikiana na TAMESO-T kwa kutoa kadi hizo ili kurahisisha mawasiliano kati ya wanachama waliopo katika maeneo mbalimbali nchini na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zao.

Kwa upande wake, Katibu wa TAMESO-T Wilaya ya Kongwa, Lucas Mlipu, ameishukuru Mixx by Yas kwa ushirikiano huo, akisema msaada wa kadi za mawasiliano kutoka kwa chama ni mwanzo mzuri wa ushirikiano utakaonufaisha wanachama wa chama hicho.

Naye Mwenyekiti wa Mafunzo ya Sayansi Shirikishi ya TAMESO-T, Musa Daudi, amesema matumizi ya kadi hizo za mawasiliano zitawezesha chama kufanya kazi kwa mfumo wa kisasa, kurahisisha uchangiaji wa fedha za chama, kuimarisha mawasiliano na kusaidia kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza miongoni mwa wanachama.

Sauti na Anwary Shabani.