Mimba za utotoni changamoto inayokatisha ndoto ya elimu kwa wasichana
2 October 2026, 16:11

Wazazi na wataalamu wanasisitiza umuhimu wa mawasiliano ya karibu kati ya wazazi na watoto, ili kuwawezesha kupata elimu, ushauri na msaada wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kupata mimba za utotoni.
Na Anwar Shabani.
Wazazi jijini Dodoma wametakiwa kuwa karibu na watoto wao wa kike na kuwapatia elimu pamoja na ushauri kuhusu madhara ya mimba za utotoni, ili kuwasaidia kujikinga na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Wakizungumza na Taswira ya Habari katika Mtaa wa St. Gemma jijini Dodoma, wazazi hao wamesema wamekuwa wakizungumza na mabinti zao kuhusu umuhimu wa kuepuka tamaa na tabia zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kupata mimba katika umri mdogo.
Wamesema mazungumzo ya mara kwa mara kati ya wazazi na watoto yanaweza kuwasaidia watoto kuelewa madhara ya mimba za utotoni na kuwapa nafasi ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo.
Kwa upande wake, Daktari Francis Mbwilo kutoka UMAT, amesema utoaji wa elimu kwa watoto kuhusu namna ya kujikinga na mimba za utotoni ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kwa wanaopata mimba katika umri mdogo.
Amesema elimu hiyo inaweza kusaidia kupunguza hatari zinazohusiana na mimba za utotoni, hivyo wazazi, jamii na wadau wengine wanapaswa kushirikiana katika kuwapatia watoto elimu sahihi.