Dodoma FM

Walimu wa shule za sekondari  watakiwa kuongeza kasi ya ufundishaji

11 November 2026, 17:07

Picha ni mwalimu akiwa na wanafunzi katika masomo ya vitendo. Picha na mwananchi.

Walimu wa Shule ya Sekondari Iyumbu jijini Dodoma wametakiwa kuongeza juhudi katika ufundishaji na usimamizi wa wanafunzi ili kuboresha kiwango cha ufaulu na kuhakikisha wanapata maarifa yatakayowawezesha kufikia malengo yao ya kielimu na kitaaluma.

Na Victory Chigwada.

Wito huo umetolewa na mwakilishi wa Zabibu Residence, Bw. Richard Lekan, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya nane ya shule hiyo, akisema taifa linahitaji wataalamu katika sekta mbalimbali, hivyo ni muhimu walimu kwa kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na kufanya vizuri katika masomo yao.

Bw. Lekan ameguswa na changamoto zinazoikabili shule hiyo, zikiwemo ukosefu wa uzio, vifaa vya michezo na maktaba ya kisasa, ambapo ametoa mchango wa shilingi milioni mbili kusaidia juhudi za kukabiliana na changamoto hizo. Aidha, amekabidhi seti mbili za jezi kwa ajili ya kuimarisha shughuli za michezo shuleni hapo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Iyumbu amesema takwimu za matokeo ya wanafunzi kwa kipindi cha miaka minne zinaonesha kuwa wanafunzi wanne walipata daraja la kwanza, 29 daraja la pili, 44 daraja la tatu, 133 daraja la nne na wanafunzi wanne walipata daraja sifuri. Takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha ufundishaji na usimamizi wa wanafunzi ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika miaka ijayo.

Simulizi na Victory Chigwada.