Wazazi watakiwa kuepuka malezi yenye vitisho, matusi
12 November 2026, 16:35

Wazazi na walezi wametakiwa kutumia mazungumzo, ushauri na mwongozo katika malezi ili kuwajenga watoto wenye kujiamini, nidhamu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Na Daniel Njau.
Matumizi ya adhabu kali kwa watoto majumbani na shuleni yametajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri ukuaji wao wa kimwili na kisaikolojia, huku wazazi, walezi na walimu wakihimizwa kutumia mbinu mbadala za malezi na utoaji wa nidhamu zinazozingatia haki na ustawi wa mtoto.
Akizungumzia suala hilo, Mwanasaikolojia Bwana Sabas Massawe amesema si lazima mtoto aadhibiwe kwa kupigwa viboko au kutukanwa anapokosea, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kumsababishia majeraha ya mwili, hofu na athari za kisaikolojia zinazoweza kuathiri mwenendo wake katika maisha ya kila siku.
Amesema wazazi na walezi wanapaswa kutumia njia chanya za kumwelekeza mtoto kwa kumweleza kosa alilofanya, kumfundisha matokeo ya matendo yake na kumpa nafasi ya kujifunza kutokana na makosa, badala ya kutumia vitisho na adhabu zinazoweza kumjengea hofu na kumfanya ashindwe kujieleza kwa uhuru.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wamesema adhabu kali hazimsaidii mtoto kujenga uelewa wa kutofautisha mema na mabaya, bali zinaweza kumfanya awe mwoga, ajitenge na kushindwa kuwaeleza wazazi, walezi na walimu changamoto zinazomkabili.