Dodoma FM

Umbali wa shule watajwa kukwamisha elimu ya wasichana Bumira

22 October 2026, 16:53

wanafunzi wa Kijiji cha Bumira hulazimika kutembea umbali wa kilomita 16 kila siku kwenda na kurudi shuleni.Picha na Dodoma fm.

Ujenzi wa shule ya sekondari katika Kijiji cha Bumira unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa elimu na kutoa fursa sawa kwa watoto wa eneo hilo kuendelea na masomo yao.

Na Stephen Noel.

Umbali mrefu kutoka Kijiji cha Bumira hadi shule ya sekondari  Kimagai umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazochangia baadhi ya wanafunzi, hususan wasichana, kukatisha masomo kutokana na uchovu na ugumu wa safari za kila siku.

Wakizungumza kuhusu changamoto hiyo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wameiomba Serikali kuwajengea shule ya sekondari ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu na kuongeza fursa za watoto, hasa wa kike, kuendelea na masomo.

George Kauya, mzee wa kijiji hicho, anasema wanafunzi wa Kijiji cha Bumira hulazimika kutembea umbali wa kilomita 16 kila siku kwenda na kurudi shuleni, hali inayoweza kuathiri mahudhurio yao na kuwakosesha mazingira rafiki ya kujifunza.

Amesema changamoto hiyo inahitaji hatua za haraka kwa kuwa umbali mrefu unaweza kuwa kikwazo kwa wanafunzi kuendelea na masomo yao, hivyo akaiomba Serikali kuweka kipaumbele katika ujenzi wa shule ya sekondari kijijini hapo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lupeta, Sopspeter Mdokho, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa kuna mipango ya kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari kwa kushirikiana na wananchi.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ni muhimu katika kutatua changamoto hiyo na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kusoma katika mazingira yanayorahisisha upatikanaji wa elimu.

Wakazi wa Bumira wanatarajia kuwa utekelezaji wa mpango huo utasaidia kupunguza umbali wa safari za wanafunzi, kuboresha mahudhurio shuleni na kupunguza hatari ya watoto, hususan wasichana, kukatisha masomo kutokana na changamoto za usafiri.

Ripoti ya Stephen Noel.