Wananchi wilaya ya Chamwino wahimizwa kudumisha usafi wa mazingira
3 November 2026, 16:43

Wananchi wametakiwa kutokufanya usafi kwa mazoea ya kusubiri kuhamasishwa pekee, bali kuufanya kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku katika maeneo ya makazi na biashara, ili kudumisha afya za jamii na kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi, salama na lenye mazingira bora kwa wote.
Na Anwary Shabani.
Wananchi wa Kata ya Chamwino, Jijini Dodoma, wametakiwa kuimarisha utamaduni wa kufanya usafi wa mazingira kila siku ili kujikinga na magonjwa yanayotokana na uchafu pamoja na kuboresha mandhari ya makazi na maeneo ya biashara.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa taka Ngumu wa Jiji la Dodoma, Bw.Mkana Mkana, wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililowakutanisha wananchi katika Kata hiyo, likiwa na lengo la kujenga jamii yenye mazingira safi na salama.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkana amesema mazingira machafu ni chanzo cha magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababisha wananchi kutumia muda na fedha nyingi kutafuta matibabu, badala ya kujikita katika shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wao wakazi wa Chamwino wamesema hali ya usafi imeendelea kuimarika kutokana na ushiriki wa wananchi, huku wakiipongeza Serikali kwa kuhamasisha zoezi hilo.

Wamesema wamefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika zoezi hilo, kwani ushiriki wa jamii katika kufanya usafi mara kwa mara ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya makazi na kupunguza hatari ya magonjwa.
Wananchi wametakiwa kutambua kuwa usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi na mwananchi atakae kiuka atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini ya shilingi 300,000 au kifungo kwa mujibu wa sheria.