Dodoma FM

Watanzania kunufaika na miradi ya Habitat for Humanity

6 October 2026, 17:20

Picha ni Bi Jacqueline utoka Habitat for Humanity International, Ofisi ya Nairobi akiwa na issa ambaye ni mnufaiaka wa huduma hiyo. Picha na Anwary Shabani.

Na AnwaryShabani.

Shirika la Habitat for Humanity International limesema limeridhishwa na utekelezaji wa miradi yake nchini Tanzania, likieleza kuwa miradi hiyo imeendelea kuboresha maisha ya wananchi kupitia ujenzi wa nyumba bora, kilimo cha kisasa, upatikanaji wa maji safi na kuimarisha usalama wa makazi.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya Habitat for Humanity Tanzania jijini Dodoma, Jacqueline Athieno kutoka Habitat for Humanity International, Ofisi ya Nairobi, amesema amefurahishwa na kuona kwa vitendo matokeo ya miradi hiyo, ambayo awali alikuwa akifuatilia kupitia picha na taarifa zilizokuwa zikitumwa kutoka Tanzania.

Picha ni nyumba ya mnufaika wa mradi wa Habitat for Humanity. Picha na Anwary Shabani.

Amesema ziara hiyo imempa fursa ya kujionea namna mradi wa kilimo cha kisasa unavyowanufaisha wananchi, ambapo katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, mradi mmoja umeweza kuwafikia moja kwa moja zaidi ya watu 88 na kunufaisha wanafunzi zaidi ya 300.

Amesema kilimo hicho kimekuwa na mchango mkubwa kwa wanafunzi, ambao hupata chakula kutokana na mazao yanayozalishwa katika mashamba ya mradi, huku pia wakipata fursa ya kujifunza kilimo na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Picha ni Bi Jacqueline kutoka Habitat for Humanity International, akionesha moja ya mazao yanayolomwa na wanufaika. Picha na Anwary Shabani.

Aidha, amesema ameguswa na miradi ya ujenzi wa nyumba inayolenga familia zenye uhitaji, wakiwemo watoto yatima na makundi mengine yanayokabiliwa na changamoto za makazi.

Kwa upande wake, Issa, ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo, ameiomba Serikali kuendelea kuiunga mkono Habitat for Humanity Tanzania ili shirika hilo liweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia miradi ya ujenzi wa nyumba, upatikanaji wa maji, usafi wa mazingira, kilimo, ufugaji na uwezeshaji wa vijana.

Simulizi na Anwary Shabani.