Mfumo dume watajwa kikwazo cha ushiriki wa wanawake katika maendeleo
24 November 2026, 17:10

Jamii imetakiwa kuondokana na mfumo dume na kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume wanapewa fursa sawa za kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
Na Victory Chigwada.
Wito huo umetolewa na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Chamwino, ambao wamesema ni muhimu kumjengea uwezo mtoto wa kike ili aweze kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kupata nafasi sawa na mtoto wa kiume.
Wamesema usawa huo utasaidia wanawake kupata nafasi ya kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu uzalishaji mali, afya ya uzazi pamoja na shughuli za kiuchumi na utafutaji wa kipato.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Kata ya Ng’hambaku, Richard Kisubi, amesema bado mwitikio wa kuwashirikisha wanawake na wasichana katika masuala mbalimbali ya kijamii ni mdogo kutokana na kuwepo kwa dhana potofu kuwa nafasi ya mwanamke ni kukaa nyumbani na kulea watoto.