Watumiaji dawa za kulevya wageukia dawa tiba zenye asili ya kulevya
6 November 2026, 17:16

Mapambano dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la mamlaka pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa familia na jamii kwa ujumla.
Na Anwary Shaban.
Udhibiti wa uingizaji wa dawa za kulevya nchini, hususan heroin, umeibua changamoto mapya baada ya baadhi ya watumiaji kugeukia matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya zinazopatikana hospitalini.
Hali hiyo imeelezwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuwa watumiaji wapo katika hatari zaidi ya kiafya.
Changamoto hiyo imebainishwa jijini Dodoma na Afisa Mwandamizi wa DCEA, Said Madadi, wakati akitoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa wafanyabiashara na wananchi katika eneo la Machinga Complex, akieleza namna mabadiliko ya upatikanaji wa dawa hizo yanavyoibua aina nyingine za matumizi hatarishi.
Katika kuendeleza mapambano hayo, Kaimu Kamishna wa DCEA Kanda ya Kati, Anna Tengie, amesema mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha operesheni za kudhibiti uzalishaji, biashara, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya, akieleza kuwa tatizo hilo linachangia vitendo vya uhalifu na kuathiri ustawi wa jamii.
Kwa upande wao, Juma Banka na Frank Ndalu, ambao ni miongoni mwa wanufaika wa elimu hiyo, wamesema wameamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya na kutoa wito kwa jamii kushirikiana na DCEA katika mapambano hayo.
Wamesimulia pia madhila waliyopitia wakati wa matumizi ya dawa hizo, ikiwemo kupoteza heshima na kujikuta wakifanya vitendo visivyo vya kawaida mbele ya familia zao, kama kujisaidia haja ndogo mbele ya wazazi wao.
Wito umetolewa kwa wananchi kutambua kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya si jukumu la mamlaka pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa familia na jamii kwa ujumla, huku wanaokumbwa na tatizo hilo wakihimizwa kutafuta msaada wa kitaalamu ili kurejea katika maisha yenye afya na heshima.