Serikali kuendelea kuimarisha tahadhari dhidi ya Ebola
18 June 2026, 17:56

Wananchi wametakiwa kuendelea kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na kutoa taarifa mapema wanapobaini mtu mwenye dalili zinazofanana na Ebola ili kusaidia juhudi za Serikali za kulinda afya za Watanzania.
Na Anwary Shaban.
Serikali imeendelea kuimarisha hatua za tahadhari na utayari wa kukabiliana na tishio la ugonjwa wa Ebola ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Waziri wa Afya Mhe. Mchengerwa amesema kutokana na mwingiliano mkubwa wa shughuli za kijamii na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani, Serikali imeamua kuchukua hatua za mapema za kuzuia na kudhibiti tishio lolote la ugonjwa huo kabla halijaleta madhara kwa wananchi.
Amesema miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kuimarisha ufuatiliaji katika mipaka ya nchi, viwanja vya ndege, bandari na maeneo mengine ya kuingilia wasafiri, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa wasafiri wote wanaoingia nchini kuzingatia kanuni za afya za kimataifa kwa kufuata taratibu za uchunguzi na upimaji zinazowekwa na mamlaka husika, ili kubaini mapema iwapo kuna mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usalama wa afya ya wananchi na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama dhidi ya magonjwa ya milipuko yanayoweza kuvuka mipaka.