Dodoma FM

Kiteto Sekondari yatekeleza matumizi ya nishati safi

15 April 2026, 5:53 pm

Mradi huu wa jiko hilo sanifu umegharimu zaidi ya shilingi milioni 63.Picha na Kitana Hamis.

Kamati hiyo pia ilitoa rai kwa Halmashauri kuhakikisha teknolojia hiyo ya nishati safi inasambazwa katika shule nyingine zote wilayani humo ili kuongeza ufanisi na kulinda mazingira kwa kiwango kikubwa zaidi.

Na Kitana Hamis.

Shule ya Sekondari Kiteto imeandika historia mpya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara baada ya kuwa shule ya kwanza kutumia jiko la kisasa linalotumia gesi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali ya Awamu ya Sita la kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi kupitia matumizi ya nishati mbadala.

Mafanikio hayo yamebainika, wakati Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ilipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.

Mradi wa jiko hilo sanifu umegharimu zaidi ya shilingi milioni 63, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri kwa kushirikiana na shule husika.

Mradi huu, unachangia kuhifadhi mazingira, kulinda afya za wapishi dhidi ya moshi.Picha na Kitana Hamis.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Hamisi Kilimo, aliusifu mradi huo na kuutaja kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa sera ya serikali.

Aidha, wajumbe wa kamati hiyo walieleza kuridhishwa na mradi huo, wakibainisha kuwa unachangia kuhifadhi mazingira, kulinda afya za wapishi dhidi ya moshi, pamoja na kuwezesha wanafunzi kupata chakula bora na kwa wakati.