Serikali yaanzisha malipo ya awali kwa wakulima wanao uza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani
20 May 2026, 12:58

Kupitia mauzo hayo, wakulima wamepata zaidi ya shilingi bilioni 82.9 tangu mwaka 2024 hadi sasa.
Na Yussuph Hassan
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwepo malipo ya awali kwa ajili ya kuwalipa wakulima wanaopeleka na kuuza mazao yao kwa mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili kuondokana na kero ya kukopwa mazao yao.
Ametoa kauli hiyo kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Stakabadhi za Ghala yanayofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu amesema kupitia mjadala uliofanyika kati ya bodi hiyo na wadau wameazimia mambo makuu matatu ili kuimarisha utendaji kazi wake na kuongeza tija kwa wakulima.
Pia ametaja kuwa wameazimia kuwa na uzingatiaji wa ubora wa bidhaa zinazopokelewa kwenye maghala kwa kuzingatia viwango vinavyotolewa na taasisi zinazohusika, ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Vipimo (WMA) na viwango vya kimataifa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala, wakulima mkoani humo wamefanikiwa kuuza tani 46,733 za mazao mbalimbali yakiwemo ufuta, dengu na mbaazi.
Senyamule amesema kupitia mauzo hayo, wakulima wamepata zaidi ya shilingi bilioni 82.9 tangu mwaka 2024 hadi sasa, na kuongeza kuwa mkoa utaendelea kuimarisha na kuendeleza matumizi ya mfumo huo ili kuongeza tija kwa wakulima.