Dodoma FM

Vilindoni jina lililobeba historia ya vihenge vya jadi Dodoma

12 June 2026, 13:06

Picha ni maghala ya kisasa yanayo patika katika baadhi ya mikoa hapa nchini.

Licha ya ukuaji wa Jiji la Dodoma na mabadiliko ya kiuchumi yanayoendelea kushuhudiwa, Vilindoni bado imehifadhi sehemu ya utambulisho wake wa kihistoria.

Na Yussuph Hassan.

Pembezoni mwa Jiji la Dodoma, ndani ya Kata ya Mbabala, kuna mtaa unaobeba simulizi ya kipekee ya historia na urithi wa jamii za zamani.

Mtaa huo ni Vilindoni. Wazee wa eneo hili husimulia kuwa jina la Vilindoni limetokana na “vilindo” — maghala ya jadi yaliyotumika kuhifadhi nafaka baada ya mavuno. Vilindo hivyo vilikuwa nguzo muhimu ya maisha ya wananchi, vikihakikisha usalama wa chakula wakati wa ukame na misimu migumu.

Leo, ingawa nyakati zimebadilika na maendeleo yamefika, jina la Vilindoni linaendelea kubeba kumbukumbu za hekima, juhudi na utamaduni wa watu walioishi na kulima katika ardhi hii kwa vizazi vingi.

Historia ya Vilindoni inaonesha kuwa eneo hili limekuwepo kwa muda mrefu kama makazi ya watu waliotegemea kilimo na ufugaji kwa maisha yao ya kila siku. Miongoni mwa alama muhimu za historia yake ni Shule ya Msingi Vilindoni, moja ya taasisi kongwe katika eneo hilo, iliyoanzishwa mwaka 1975.

Uwepo wa shule hiyo unaashiria kuwa kufikia miaka ya 1970, Vilindoni ilikuwa tayari imejengeka kama jamii yenye wakazi wa kudumu na mahitaji ya huduma za kijamii, hususan elimu kwa watoto.

Kwa wakazi wa zamani, shule hiyo haikuwa tu mahali pa kujifunzia kusoma na kuandika, bali ilikuwa kitovu cha maendeleo ya jamii. Vizazi vingi vya watoto kutoka Vilindoni na maeneo jirani vimepata elimu yao ya msingi hapo, na wengi wao wamekua kuwa viongozi, watumishi wa umma, wafanyabiashara na wataalamu katika nyanja mbalimbali. Hivyo, historia ya Vilindoni haiwezi kutenganishwa na historia ya shule hiyo ambayo imeendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya wananchi.

Simulizi za vilindo vya kuhifadhia nafaka, pamoja na uwepo wa taasisi za muda mrefu kama Shule ya Msingi Vilindoni, ni ushahidi wa safari ndefu ya maendeleo ya eneo hili kutoka jamii za wakulima wa zamani hadi kuwa sehemu ya Dodoma ya kisasa. Ni historia inayostahili kuhifadhiwa na kusimuliwa ili vizazi vya sasa na vijavyo viweze kufahamu chimbuko na urithi wa mahali wanapoishi.