Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 70 katika sekta ya usafiri nchini
3 August 2026, 17:51

Uwekezaji huo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya usafiri kwa kuzalisha wataalamu wenye ubora watakaochangia maendeleo ya uchumi wa Taifa na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Na mwandishi wetu.
Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 70 katika sekta ya usafiri nchini kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukuza uchumi hadi kufikia dola trilioni moja.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari, Mtumba jijini Dodoma, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dkt. Prosper Mgaya, amesema uwekezaji huo umefanyika kupitia Mradi wa Umahiri wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), hususan katika eneo la usafiri wa anga.
Dkt. Mgaya amesema mradi huo umeiwezesha NIT kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuongeza uwezo wa chuo kuandaa wataalamu wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi viwango vya kimataifa, ili waweze kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.