Miundombinu salama ya hedhi ipewa kipaumbele shuleni
23 September 2026, 16:45

Baadhi ya wananchi wamesema afya na usafi wa hedhi vinapaswa kupewa kipaumbele na jamii nzima, kwa kuhakikisha wasichana wanapata vifaa salama na vya kutosha vya kujisitiri, pamoja na elimu sahihi itakayowawezesha kuelewa na kusimamia hedhi zao kwa usalama, heshima na kujiamini.
Na Irene Robert.
Upatikanaji wa miundombinu salama ya kujisitiri pamoja na vifaa vya hedhi ni muhimu katika kukuza usawa wa kijinsia katika elimu, huku hatua hiyo ikisaidia kuondoa vikwazo vya kisaikolojia na kimwili vinavyoweza kuchangia utoro wa wanafunzi wa kike shuleni.
Hayo yameelezwa na Catherine Kalinga, Mkurugenzi wa Shirika la Kuwasaidia Wanawake, Wasichana na Vijana (GAET), wakati akizungumza na KM24 FM, ambapo amesisitiza umuhimu wa jamii kuhakikisha wasichana wanapata mahitaji muhimu pamoja na elimu sahihi kuhusu afya na usafi wa hedhi.
Kwa upande wake, Agness Mkanga, Mkufunzi wa Afya ya Uzazi na Hedhi Salama kutoka Hospitali ya Manispaa ya Kahama, ameeleza changamoto zinazoweza kutokana na kutokuwa na mazingira salama wakati wa hedhi, huku akieleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata usaidizi pamoja na mahitaji muhimu wanayohitaji katika kipindi hicho.
Kwa ujumla, jamii imetakiwa kuhakikisha wasichana wanapata elimu sahihi kuhusu hedhi, pamoja na vifaa vya kujisitiri, maji safi, sabuni na vyoo salama vyenye faragha ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku, ikiwemo masomo, kwa mazingira salama na yenye heshima.