Serikali yaandaa marekebisho ya sheria ya ndoa
28 September 2026, 16:34

Hatua hiyo inaendelea kuhitaji ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali, kwa lengo la kulinda haki za watoto wa kike, kuwawezesha kuendelea na elimu na kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao.
Na Anwary Shaban.
Serikali imesema ipo katika hatua za mashauriano ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Ndoa, hususan vinavyohusiana na masuala ya elimu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kushughulikia changamoto ya ndoa za utotoni nchini.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kushughulikia suala la ndoa za utotoni, ikiwemo kupitia upya baadhi ya vifungu vya sheria vinavyohusiana na masuala hayo amesema wakati akizungumza katika Programu Maalumu ya Sema na Waziri.
Aidha, Waziri Homera amesema Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana na Plan International katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki na fursa ya kupata elimu na kutimiza ndoto zake.
Ametoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia mabinti wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali, ili kuwawezesha kutumia fursa zilizopo na kujenga maisha yenye tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jane Sembuche, amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 29.1 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 walioolewa waliingia katika ndoa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Amesema hali hiyo inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa elimu, afya pamoja na fursa za kiuchumi kwa wasichana, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuchukua hatua za pamoja katika kukabiliana na ndoa za utotoni.