Kituo cha afya Makole kimepokea vifaa tiba vya usonji kutoka AMREF
23 October 2026, 17:02

Ushirikiano wa NBC na AMREF unalenga kuimarisha huduma za afya ya msingi na kuwafikia watoto wenye mahitaji maalumu, huku uwekezaji zaidi ukihitajika ili vituo vingine vya afya katika Jiji la Dodoma viweze kutoa huduma hizo.
Na. Anwary Shabani.
Kituo cha Afya Makole, Jiji la Dodoma, kimepokea vifaa tiba kutoka Shirika la Afya na Utafiti la Afrika (AMREF) kwa ufadhili wa Benki ya Kitaifa ya Biashara (NBC), kwa ajili ya kuboresha huduma kwa watoto wenye usonji.
Vifaa hivyo vitasaidia kusogeza huduma karibu kwa wananchi na kupunguza usumbufu kwa wagonjwa kwenda hospitali ya mkoa wa Dodoma na kuboresha mazingira ya matibabu kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Rutachunzibwa alisema kuwa msaada huo utasaidia kuboresha huduma kwa watoto wenye usonji na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Alisema kuwa ushirikiano wa AMREF na NBC umesaidia kusogeza huduma za tiba kwa vitendo na tiba ya viungo karibu na wananchi kupitia vituo vya afya vya msingi, hatua inayopunguza usumbufu kwa familia zinazotafuta huduma hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la Afya na Utafiti la Afrika (AMREF), Dkt. Rita Mutayoba alisema kuwa ufadhili wa Benki ya Kitaifa ya Biashara (NBC) umewezesha kuanzisha juhudi za kuimarisha huduma kwa watoto wenye usonji.
Nae, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole Dkt. Revocatus Baltazary alisema kuwa kituo kilianza kutoa huduma za utengamano Julai mosi, 2026, kikiwa na wataalamu wawili wa tiba kwa vitendo na tiba ya viungo, hatua iliyosogeza huduma karibu na wananchi.

Alisema kuwa hadi sasa kituo hicho kimehudumia wateja 123 kupitia huduma za tiba kwa vitendo na tiba ya viungo, huku mafunzo yaliyotolewa kwa watumishi 10 yakisaidia kubaini watoto sita kati ya 63 waliokuwa na viashiria vya usonji.