Dodoma FM

Pumba ya mpunga yageuka fursa

24 August 2026, 18:14

Teknolojia hiyo inatarajiwa kusaidia kupunguza ukataji wa miti, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.Picha na Mtandao.

Wadau wa mradi huo wamewataka wajasiriamali na sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika teknolojia hiyo ili pumba ya mpunga itumike kama malighafi ya nishati mbadala, badala ya kutupwa na kupoteza fursa ya kuongeza thamani.

Na Anwary Shaban.

Pumba ya mpunga ambazo kwa muda mrefu imekuwa ikitupwa baada ya mavuno, sasa imeanza kugeuka kuwa fursa ya biashara kwa wajasiriamali, kupitia teknolojia ya kuibadilisha kuwa mkaa mbadala.

Teknolojia hiyo inatarajiwa kusaidia kupunguza ukataji wa miti, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika warsha ya kuhitimisha mradi wa kuongeza thamani ya pumba za mpunga kwa ajili ya kuzalisha mkaa mbadala, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Teknolojia na Viwanda kutoka SIDO, Mhandisi Kalumuna Benedicto,amesema teknolojia hiyo inaweza kutengenezwa nchini kupitia taasisi kama SIDO na TEMDO pamoja na karakana ndogo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kuongeza Thamani ya Pumba za Mpunga kwa ajili ya Kuzalisha Mkaa Mbadala kutoka UNIDO, Faustine Msangira, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za kusaidia serikali kupunguza ukataji wa miti na kuhifadhi mazingira.

Naye mnufaika wa mradi huo na mashine, Christopher Salim amesema teknolojia hiyo imewapa fursa  ya kuongeza uzalishaji na kipato, sambamba na kuunda ajira kwa vijana na wanawake.