Wahitimu wa darasa la saba na kidato cha nne wasiozeshwe
2 October 2026, 16:51

Wazazi na walezi wametakiwa kuacha kuwaozesha watoto kwa lengo la kupata fedha, akisisitiza kuwa elimu na ujuzi ni miongoni mwa nyenzo muhimu za kuwawezesha vijana kujitegemea na kuchangia maendeleo ya familia na Taifa.
Na Hamis Kitana.
Wazazi na walezi wilayani Handeni mkoani Tanga wametakiwa kutowaozesha watoto wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne, badala yake kuwapa fursa ya kuendelea na elimu, ikiwemo mafunzo ya ufundi.
Wito huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Chanika, Halmashauri ya Mji Handeni, Habibu Mbota, wakati wa mahafali ya wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) wilayani humo.
Mbota amesema wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne wanahitaji kupewa fursa ya kupata elimu na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kujenga maisha yao ya baadaye.