Dodoma FM

Mama, watoto wawili wafariki kwa moto Mpwapwa

6 October 2026, 11:40

Picha ni nyumba ikiteketea kwa moto, na zoezi la uokoaji wa samani ukiendelea. Picha na Mwananchi.

Katika hali ya huzuni familia moja imepokea msiba wa mama na watoto wake wawili kuteketea kwa moto na kwa masikitiko makubwa, huku jamii ikitakiwa kuwa makini na kuepuka kuhifadhi vitu vinavyoweza kusababisha madhara, hususan mafuta ya petroli na vifaa vingine hatarishi, ndani ya nyumba za makazi.

Na Stephen Noel.

Mama mmoja na watoto wake wawili wamefariki dunia baada ya kuteketea kwa moto ndani ya nyumba yao, huku mtoto mwingine akinusurika akiwa amejeruhiwa vibaya katika tukio la moto lililotokea usiku wa manane katika Kitongoji cha Tambuka Leri, Kijiji cha Inzomvu, Kata ya Kimagai, Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma.

Waliofariki katika tukio hilo wametajwa kuwa ni Stela Manyelezi (30) pamoja na watoto wake wawili, Veronika Martin (9) na Vivian Martin (7).

Kwa mujibu wa mashuhuda, moto huo ulianza baada ya mafuta ya petroli yaliyokuwa yakihifadhiwa ndani ya nyumba kulipuka, na kusababisha moto mkubwa ulioshindwa kudhibitiwa kwa wakati.
Mtoto mwingine, Vaileth Manyelezi (15), amenusurika katika tukio hilo akiwa amejeruhiwa vibaya na kukimbizwa kwa ajili ya kupata matibabu.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, George Manyelezi, ambaye ni baba mdogo wa Stela Manyelezi, amesema taarifa za awali zinaeleza kuwa moto huo huenda ulisababishwa na petroli kulipuka baada ya kutokea hitilafu ya umeme kutoka kwenye betri la mfumo wa sola lililokuwa ndani ya nyumba.

George amesema familia imepokea msiba huo kwa masikitiko makubwa, huku akitoa wito kwa jamii kuwa makini na kuepuka kuhifadhi vitu vinavyoweza kusababisha madhara, hususan mafuta ya petroli na vifaa vingine hatarishi, ndani ya nyumba za makazi.

Amesema tukio hilo linapaswa kuwa fundisho kwa jamii kuchukua tahadhari zaidi katika matumizi na uhifadhi wa vitu vinavyoweza kusababisha moto, ili kuzuia majanga kama hayo yasitokee tena.

Simulizi na Stephen Noel