Dodoma FM

PSPTB kuwafutia leseni wadaiwa sugu

19 October 2026, 16:38

Picha ni mkurugenzi mtendaji wa bodi ya wataalamu wa ununuzi ugavi Bw. Godfrey Mbanyi jijini Dodoma, akizungumza na waandishi wa habari.

Kutokana na mamlaka hayo ya kisheria, PSPTB imetangaza kuwa itaweka wazi orodha ya majina ya wanachama hai wa kitaaluma, ambao pekee ndio watakao stahili kufanya kazi za ununuzi na ugavi kwa mujibu wa sheria, tofauti na watu ambao hawajatimiza masharti ya kitaaluma.

Na Anwary Shabani.

Wataalamu 4,449 wa ununuzi na ugavi nchini wametambuliwa kuwa wanachama hai wa Bodi ya wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kati ya wataalamu 22,269 walio sajiliwa na bodi hiyo, huku hatua hiyo ikilenga kuhakikisha shughuli za ununuzi na ugavi zinafanywa na wataalamu wenye sifa na vibali vinavyo tambulika kisheria.

Katika taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mtendajiwa wa bodi hiyo Bw. Godfrey Mbanyi jijini Dodoma Oktoba amesema Bodi hiyo ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti viwango vya kitaaluma, mwenendo na maadili ya wataalamu wa ununuzi na ugavi nchini, kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB, Sura ya 179 ya Sheria za Tanzania.

Aidha amesema Bodi hiyo pia ina jukumu la kusajili watu wenye sifa zinazo takiwa na kuwapa mamlaka ya kufanya kazi za kitaaluma katika fani hiyo.

PSPTB imeeleza kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 38(1)(b) cha Sheria ya PSPTB ya mwaka 2009, ina mamlaka ya kumfuta mtu kwenye orodha ya wanachama endapo atashindwa kulipa ada kwa zaidi ya miezi 24.

Hadi Oktoba 15, 2026, wanachama hai walio kidhi vigezo vya kufanya kazi za ununuzi na ugavi walikuwa 4,449, sawa na sehemu ya jumla ya wataalamu 22,269 walio sajiliwa. Hatua hiyo inalenga kuimarisha uzingatiaji wa sheria, viwango vya taaluma na maadili katika sekta ya ununuzi na ugavi nchini.

Simulizi na Anwary Shabani.