Maafisa usafirishaji walalamikia mikataba, waiomba serikali kuingilia kati
16 October 2026, 16:51

Baadhi ya maafisa usafirishaji almaarufu kama bodaboda katika eneo la Kituo cha Ujenzi wilayani Mpwapwa wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto ya mikataba kati yao na wamiliki wa pikipiki, wakisema uelewa mdogo wa sheria na masharti ya mikataba unawaweka katika mazingira yanayoweza kuhatarisha haki zao.
Na Stephen Noel.
Wakizungumza katika mahojiano maalumu, waendesha bodaboda hao wamesema baadhi ya wamiliki wa pikipiki hutumia mwanya wa kutofahamu kwa kina masharti ya mikataba kwa manufaa yao, hali inayoweza kuchochea migogoro na malalamiko kati ya pande hizo mbili.
Mmoja wa waendesha bodaboda hao, Azori Mduwile, amesema ni muhimu kutolewa kwa elimu ya sheria na mikataba ili kuwawezesha waendesha bodaboda kuelewa haki na wajibu wao kabla ya kuingia katika makubaliano na wamiliki wa pikipiki.
Mduwile amezitaka mamlaka husika, hususan idara zinazoshughulikia masuala ya vijana, kuandaa programu za elimu zitakazowawezesha waendesha bodaboda kufahamu sheria zinazowaongoza na namna ya kujilinda dhidi ya mikataba inayoweza kuwaweka katika mazingira magumu.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Matlina Batholomeo, amewashauri waendesha bodaboda kutunza kumbukumbu za malipo wanayofanya pamoja na nakala za mikataba waliyoingia na wamiliki wa pikipiki.
Amesema utunzaji wa kumbukumbu hizo ni muhimu katika kutoa ushahidi na kurahisisha utatuzi wa migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuelewana kuhusu utekelezaji wa masharti ya mikataba.
Wadau hao wameeleza kuwa elimu ya sheria na mikataba ni muhimu katika kulinda haki za waendesha bodaboda na kuimarisha uhusiano kati yao na wamiliki wa pikipiki.