Dodoma FM

Umuhimu wa michezo kwa watoto katika ukuaji wao

5 November 2026, 16:01

Picha ni watoto wakiwa wanafurahia michezo mbalimbali katika muda wao waziada. Picha na UN News.

Kwa kuzingatia umuhimu wa michezo katika makuzi ya watoto, wazazi na walezi wanahimizwa kuhakikisha watoto wanapata muda wa kutosha wa kucheza huku wakisimamiwa ipasavyo, ili kunufaika na michezo hiyo katika kukuza afya, vipaji na uwezo wao wa kijamii bila kuhatarisha usalama wao.

Na Daniel Njau.

Michezo imetajwa kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji na maendeleo ya watoto, ikiwasaidia kuimarisha afya ya mwili na akili, kujenga uwezo wa kushirikiana na wenzao pamoja na kukuza vipaji. Hata hivyo, wananchi wameonya kuwa michezo hiyo inapaswa kufanyika katika mazingira salama na chini ya uangalizi wa wazazi au walezi ili kuepusha ajali na madhara yanayoweza kujitokeza.

Wananchi waliozungumza wamesema michezo huwajengea watoto uwezo wa kuwasiliana, kushirikiana na wenzao na kujifunza kuishi katika jamii, huku ikiwasaidia kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kutokana na shughuli za masomo na majukumu ya kila siku. Wamesisitiza kuwa watoto wanapaswa kupata muda wa kutosha wa kucheza kama sehemu ya makuzi yao.

Hata hivyo, wameeleza kuwa baadhi ya michezo inaweza kuhatarisha usalama wa watoto, hasa inapofanyika katika maeneo yasiyofaa au bila uangalizi wa watu wazima. Wamewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawasimamia watoto wakati wa michezo ili kuwalinda dhidi ya ajali na kuwawezesha kufurahia shughuli hizo katika mazingira salama.

Kwa upande wake, mlezi katika kituo cha watoto cha World Vision Bi Magreth Msaki amesema michezo ni nyenzo muhimu katika kukuza maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili na kijamii. Amehimiza wazazi na walezi kuwatengea watoto muda wa kucheza na kujumuika na wenzao baada ya kukamilisha masomo na majukumu ya nyumbani, akieleza kuwa kufanya hivyo huwasaidia kukuza vipaji, kuimarisha afya na kujenga kujiamini.

Simulizi na Daniel Njau.