Nini kinapelekea wenza kufikia hatua ya kutoana uhai
2 November 2026, 16:32

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa wanandoa kujenga utamaduni wa mawasiliano yenye afya, kutafuta ushauri wa kitaalamu wanapokabiliwa na changamoto na kuchukua hatua za kujilinda pale dalili za ukatili zinapojitokeza, ili kuzuia migogoro isigeuke kuwa chanzo cha kupoteza maisha.
Na Mwanaidi Mpetu.
Migogoro ya ndoa inayochochewa na wivu, kushindwa kuelewana pamoja na changamoto za kimawasiliano inatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri ustawi wa familia, huku baadhi ya migogoro hiyo ikifikia hatua ya kusababisha vitendo vya ukatili na hata mauaji baina ya wenza.
Wakizungumza kuhusu hali hiyo, baadhi ya wananchi wameeleza kuwa wivu uliopitiliza, kutokuaminiana na kushindwa kusuluhisha tofauti zinazojitokeza ndani ya ndoa ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuongeza migogoro baina ya wenza.
Kwa upande wake, mwanasaikolojia kutoka hospitali ya afya ya akili Mirembe Jijini Dodoma Dkt Arapha anaeleza kuwa kushindwa kudhibiti hisia, hasira, wivu uliopitiliza pamoja na kukosekana kwa mbinu sahihi za kutatua migogoro kunaweza kuongeza hatari ya vitendo vya ukatili ndani ya mahusiano.