Dodoma FM

Kukata tamaa kunavyochochea baadhi ya watu kujidhuru

19 November 2026, 16:45

Picha ni mwanaume anayeonekana akiwa na msongo wa mawazo uliopitiliza, Picha na Mwananchi.

Hali ya kukata tamaa na kukosa matumaini katika maisha imeendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri ustawi wa afya ya akili katika jamii, huku baadhi ya watu wakifikia hatua ya kuwaza kujidhuru kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Na Daniel Njau.

Wakizungumzia hali hiyo, wananchi wamesema changamoto za maisha, migogoro ya kifamilia na kukosekana kwa mtu wa kuzungumza naye ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza hali ya kukata tamaa, hivyo kuitaka jamii kujenga utamaduni wa kusikilizana, kusaidiana na kutowahukumu watu wanaopitia nyakati ngumu.

Wananchi wameeleza umuhimu wa kuimarishwa kwa elimu ya afya ya akili ili kusaidia jamii kutambua na kuwafikia mapema watu wenye changamoto hizo.

Akifafanua kuhusu hali hiyo, mtaalamu wa saikolojia, Dkt. Faustine China, amesema mawazo ya kujidhuru yanaweza kuchangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo za kisaikolojia, kijamii na kibaiolojia, huku akibainisha kuwa dalili zinazopaswa kupewa uzito ni pamoja na mabadiliko ya tabia, hasira za mara kwa mara, kujitenga na wengine, kukata tamaa na kauli zinazoashiria kutokuwa na hamu ya kuendelea kuishi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa familia na jamii kuwapa nafasi watu wanaoonyesha dalili hizo kueleza hisia zao, kuwafariji na kuwasaidia kupata huduma za kitaalamu badala ya kuwatenga au kuwahukumu, huku akieleza kuwa msaada wa mapema unaweza kusaidia kuzuia madhara makubwa.

Ameongeza kuwa elimu ya afya ya akili inapaswa kuendelea kutolewa mijini na vijijini ili kujenga jamii yenye uelewa na utayari wa kusaidiana.

Ripoti ya Daniel Njau.