Vijana wahimizwa kutumia kilimo cha mbogamboga, matunda kujiajiri
15 October 2026, 17:08

Katika jamii ya vijana inayosubiri ajira kwa wingi wamewahimiza kutafuta na kutumia fursa zilizopo katika kilimo, iwe kwa kujiunga katika vikundi au kufanya shughuli hizo mmoja mmoja, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi na kujenga maisha bora ya baadaye.
Na Daniel Njau.
Wakati ukosefu wa ajira ukiendelea kuwa changamoto kwa vijana, kilimo kinatajwa kuwa miongoni mwa fursa zinazoweza kuwawezesha kujiajiri, kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi badala ya kusubiri ajira za kuajiriwa.
Kijana Jumanne Iddi ni miongoni mwa vijana walioamua kutumia fursa hiyo kwa kujikita katika kilimo cha mboga na matunda ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku, huku akilenga kuhamasisha vijana wengine kutambua na kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo.
Iddi amesema mafanikio katika kilimo yanategemea kufuata kanuni bora za uzalishaji ili kupata mazao mengi na yenye ubora. Aidha, amesisitiza umuhimu wa wakulima kupata elimu ya kilimo itakayowawezesha kutumia mbinu sahihi na kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesema awali alisomea uandishi wa habari, lakini baada ya kumaliza masomo yake aliamua kujikita katika kilimo baada ya kutambua kuwa kinaweza kuwa chanzo cha kipato na kumwezesha kujitegemea bila kusubiri ajira.