Dodoma FM

Serikali kuendelea kuimarisha huduma waathirika wa matukio ya ukatili

27 October 2026, 17:55

Picha ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhandisi Maryprisca Mahundi, wakati wa kipindi cha maswali na majibu.Picha na Bunge.

Mahundi amewahimiza wananchi kuripoti matukio ya ukatili huo kupitia namba ya dharura ya Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi, 0699 913200, au namba 116, inayopatikana wakati wote.

Na Mariam Kasawa.

Serikali imelaani vitendo vya ubakaji na ukatili wa kijinsia, ikisema inaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria na huduma kwa waathirika, huku ikiwataka wananchi kuripoti matukio hayo na kushirikiana na vyombo vya dola.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma, leo Oktoba 27, 2026, na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhandisi Maryprisca Mahundi, wakati wa kipindi cha maswali na majibu, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma, aliyetaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu matukio ya ubakaji yanayosababisha waathirika kupata ujauzito.

Mahundi amesema Serikali inaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazomlinda mtoto dhidi ya makosa ya ukatili, yakiwemo ubakaji na ulawiti.

Ameeleza kuwa kuanzia Januari hadi Desemba 2025, jumla ya makosa 7,219 ya ubakaji yaliripotiwa na kushughulikiwa.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na ukatili huo, pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa waathirika kupitia Ofisi za Ustawi wa Jamii, Madawati ya Jinsia na Watoto ya Jeshi la Polisi na Ofisi za Serikali za Mitaa.

Sauti ya Mhandisi Maryprisca Mahundi,