Wananchi watakiwa kuwa makini matumizi ya vifaa ya umeme kuepuka majanga ya moto
22 September 2026, 16:58

Kwa kuzingatia kuwa moto unaweza kutokea wakati wowote na kusababisha hasara kubwa kwa maisha na mali, elimu, tahadhari na maandalizi ya mapema vinaendelea kuwa muhimu kwa kila mwananchi.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini Dodoma limewataka wananchi kuongeza umakini katika matumizi ya vifaa vya umeme na gesi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia majanga ya moto yanayoweza kutokea katika maeneo ya biashara na makazi.
Jeshi hilo limeendelea kutoa elimu na ushauri kwa wananchi kuhusu hatua mbalimbali za kuchukua ili kujikinga na majanga ya moto, pamoja na namna ya kukabiliana na moto unapozuka.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Ofisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Christian Lalika, amesema wananchi wanapaswa kuhakikisha vifaa vya umeme vinakaguliwa mara kwa mara, hususan wafanyabiashara wanaotumia umeme katika vibanda vya simu.
Amesema pia wananchi wanaotumia gesi kwa ajili ya kupikia wanapaswa kuwa makini wakati wa matumizi na kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumiwa kwa usahihi.
Aidha, Lalika amewataka wananchi kujifunza namna sahihi ya kutumia vifaa vya kuzimia moto, akieleza kuwa uelewa huo unaweza kusaidia kudhibiti moto katika hatua za awali kabla haujasambaa na kusababisha madhara makubwa.
Amesema hatua za haraka na matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto vinaweza kusaidia kupunguza ukubwa wa janga na kulinda maisha pamoja na mali.
Katika kuangalia namna wananchi wanavyotekeleza tahadhari hizo, Taswira ya Habari imezungumza na baadhi ya wafanyabiashara katika eneo la Miyuji jijini Dodoma, ambapo wameeleza hatua wanazochukua katika maeneo yao ya biashara ili kuzuia au kukabiliana na moto pindi unapotokea.
Wananchi hao pia wametoa ushauri kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwa makini na vyanzo vya moto, pamoja na kuzingatia usalama wakati wa kutumia vifaa vya umeme na gesi.