Kijana wa miaka 21 ajinyonga na kuacha ujumbe wa msamaha
10 September 2026, 16:31

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chambinga, Hezron Mathias Mbeho, amesema tukio hilo limeumiza jamii kutokana na kutokea kwa kushtukiza, huku akiwataka vijana kutokaa kimya wanapokabiliwa na changamoto, bali kuzungumza na watu wanaoweza kuwasaidia, wakiwemo viongozi wa kijiji, watendaji na polisi.
Na Anwary Shabani.
Kijana mwenye umri wa miaka 21, mkazi wa kijiji cha Mpinga wilayani Bahi, amefariki dunia baada ya kukutwa amejinyonga katika eneo la shamba nyumbani kwao, baada ya kurejea kutoka Chigongwe alipokuwa akifanya kazi.
Baba wa marehemu, Augustino Wami, amesema asubuhi ya siku ya tukio walikaa pamoja kifamilia yeye na mke wake, pamoja na marehemu na mke wake, kabla ya kila mmoja kuendelea na shughuli zake.
Amesema akiwa katika shughuli za kuchunga mifugo alipokea simu kutoka nyumbani kwamba mwanawe alikuwa amemwambia mke wake amtunze mtoto wao kwa kuwa hatamuona tena, na alipofuatilia alikuta tayari amefariki.
Baada ya polisi na daktari kufika eneo la tukio, walielezwa kukuta marehemu ameacha ujumbe wa maandishi akiomba msamaha kwa mtu yeyote ambaye huenda alimkosea, huku akisema amewasamehe pia wale waliomkosea.