Dodoma FM

Taasisi zatakiwa kuongeza ubunifu ili kuleta mageuzi sekta ya kilimo

29 March 2021, 10:02 am

Na; Rabiamen Shoo.

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amezitaka Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kuongeza ubunifu ili kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo sambamba na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda na kilimo nchini.

Akizungumza baada ya kuzindua mradi unaolenga kuvutia na kuwahamasisha wanaohitimu vyuo kujikita katika kilimo biashara mkoani Morogoro, Profesa Mkenda amesema mageuzi katika sekta ya kilimo yatasaidia kupunguza umaskini miongoni mwa Watanzania.

Profesa Mkenda ametoa Mwito kwa benki ya biashara na taasisi nyingine za kifedha kutoa mikopo yenye masharti na nafuu kwa vijana wanaojishughulisha na kilimo biashara ili kuharakisha mageuzi katika sekta ya kilimo.

Makamu Mkuu wa Chuo SUA, Profesa Raphael Chibunda amesema chuo kitaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kusukuma na kuubadilisha mfumo wa kilimo ili wakulima wajikite katika kilimo biashara.