Dodoma FM

Mnada wa Dabalo wakabiliwa na ukosefu wa matundu ya vyoo

31 August 2021, 11:56 am

Na; Beanrd Filbert.

Ukosefu wa matundu ya vyoo katika mnada wa Dabalo kata ya Dabalo wilayani Chamwino imetajwa kuwa changamoto kwa wafanyabiashara hali inayoweza kuhatarisha afya zao.

Hayo yameelezwa na Diwani wa kata ya Dabalo Bwana Isihaka Rajab wakati akizungumza na taswira ya habari kuhusu matundu ya vyoo yaliyopo katika eneo ambapo mnada unafanyika kama yanajitosheleza na kukidhi mahitaji ya watu.

Bwana Isihaka amesema mnada huo umekuwa na mkusanyiko wa watu wengi lakini bado kuna changamoto ya matundu ya vyoo ambapo mpaka hivi sasa kuna matundu 4 pekee na kati ya hayo ni 2 wanaume na 2 wanawake.

Bwana Rajab ameongeza kuwa tayari halmashauri ya Chamwino imetenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika bajeti ya mwaka 2021/22 na hivi karibuni utekelezaji utaanzaa.

Mnada unaokutanisha wafanyabiashara mbalimbali katika kata ya Dabalo wilayani chamwino unafanyika kila jumapili ya mwisho wa mwezi ambapo unakadiriwa kukusanya mapato zaidi ya milioni 2 kwa kila mwezi.