Dodoma FM

Wakazi wa kijiji cha Nholli kuanza ujenzi wa zahanati

19 July 2021, 10:35 am

Na; Victor Chigwada.

Wakazi wa kijiji cha Nholi kata ya Mpalanga wilayani Bahi wamekabidhiwa mifuko miatatu ya saruji kwaajili ya ujenzi wa zahanati.
Wakizungumza na taswira ya habari wakazi wa kijiji hicho wamemshukuru mbunge wa jimbo la Bahi mh. Kenneth Nollo kwa kutimiza ahadi aliyoitoa kipindi cha kampeni ya kuhakikisha kijiji hicho kina pata zahanati.

Nae Diwani wa Kata ya Mpalanga Bw.Baraka Ndahani amekiri mbunge huyo kufanya ziara katika kijiji hicho ambapo alifanikiwa pia kutimiza ahadi yake kwa wanakijiji wa Nholi na kuwapatia mifuko 300 ya saruji licha ya kuwa walishaanza ufyatuaji wa matofali.

Akizungumza katika ziara hiyo Mh.Noll amewahakikishia wananchi kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu tayari ujenzi wa zahanati utakuwa umefikia hatua nzuri huku akiwapongeza wananchi kwa ushiriki wao katika kazi za ujenzi wa zahanati.

Nollo amemengeza kuwa licha ya ujenzi huo bado anatarajia kuanzisha ujenzi wa zahanati nyingine eneo la mgodini ili kuhakikisha huduma za afya zinasogea karibu na wananchi.

Viongozi mbalimbali wameendelea kuboresha huduma za jamii ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo.