Dodoma FM

Masinyeti waomba Serikali iwasaidie kujenga zahanati

29 July 2021, 11:25 am

Na; Alfred Bulahya.

Idilo , Mpwapwa walia na ukosefu wa huduma ya Afya – Dodoma FM

Wananchi wa kijiji cha masinyeti Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuwaunga mkono katika ujenzi wa zahanati ya kijiji ili kuwezesha kupata huduma za afya kijini hapo.

Hayo yamebainishwa na wakazi wa kijiji hicho wakati wakizungumza na taswira ya habari na kusema kuwa Kijiji hicho hakina zahanati tangu kilipoanzishwa miaka 9 iliyopita hali inayowafanya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

Wamesema katika kukamilisha ujenzi huo wameanza kwa kuchangia michango mbalimbali ili kufanikisha zoezi hilo na kuiomba Serikali kuwaunga mkono ili kupatikana kwa zahanati hiyo na huduma zianze kutolewa.

Afisa mtendaji wa Kijiji hicho Bi. Ashura Elinihaki amesema kuwa ni kweli ukosefu wa zahanati kijijini hapo unachangia kurudisha nyuma maendeleo kutokana na wananchi kutumia muda mrefu na gharama kubwa kupata huduma za afya katika vijiji vya jirani.

Pamoja na hayo amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuchangia michango mbalimbali inayolenga kukamilisha ujenzi huo huku akiahidi kufuatilia ngazi ya Serikali kuu ili kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.