Dodoma FM

RUWASA kutatua kero ya maji katika vijiji vya Msembeta, Chigongwe, Nala, na Lugala

4 May 2021, 10:22 am

Na; Selemani kodima

Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini  wilaya ya  Dodoma umesema una mpango wa kumaliza changamoto ya maji katika maeneo ya Msembeta,Chigongwe ,Nala pamoja na Lugala kwa kutoa maji bonde la Mzakwe .

Hayo yamesemwa na Meneja msaidizi wa RUWASA wilaya ya Dodoma Mhandisi Charles Muhenjwa  wakati akielezea mkakati wa RUWASA wa kumaliza changamoto ya maji katika eneo la lugala  ambapo amesema hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na Utafiti  wa kujua ni wapi bomba zitapita na baadae kuanza usanifu.

Amesema kabla ya kufanikisha mpango wa kumaliza tatizo la maji ,wanategemea kuwa na mpango wa kutengeneza matenki ya muda mrefu ili kuachana na matumizi ya matenki ya plastiki.

Mhandisi Charles amesema kati ya mwezi 5 au 6 kupitia programu ya lipa kwa matokeo itawezesha kutoa ufumbuzi wa maeneo yote yenye changamoto ya maji hivyo wanasubiri fedha za programu hiyo ili kuanza Utekelezaji.

Pamoja na hayo amesema Mradi wa kutoa maji Mzakwe kwenda maeneo ya Msembeta,Chigongwe ,Nala pamoja na Lugala utaingizwa kwenye Bajeti ya mwaka 2022/2023 lakini iwapo fedha zitaingizwa mapema wanataraji mradi huo utafanya  kazi kwa mwaka 2021/2022.