Dodoma FM

Mahama walalamika fedha za ujenzi wa zahanati hazitoshelezi

27 November 2023, 4:43 pm

Walipokea kiasi cha fedha milioni kumi na tatu kwaajili ya umaliziaji wa zahanati hiyo. Picha na michuzi blog.

Hatua ya Ujenzi wa Mradi huo ni utekelezaji wa Wananchi kushiriki katika utatuaji wa changamoto hasa Afya ambapo Sera ya afya ya Mwaka 2007 inaelekeza kila kijiji kinatakiwa kuwa na Zahanati.

Na Victor Chigwada.

Licha ya serikali kutoa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Mahama bado inaelezwa kuwa hazitoshelezi ili kukamilisha mradi huo ambao wananchi walianza kuutekeleza .

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kijiji  hicho Bw Asheri Mkosi  wakati akizungumza na Dodoma Fm ambapo amesema kuwa baada ya kuhamasisha ujenzi wa zahanati kwa kutumia nguvu za wananchi walifanikiwa kupata fedha kutoka Serikalini lakini bado hazikutosheleza katika kukamilisha Ujenzi huo.

Amesema kuwa walipokea kiasi cha fedha milioni kumi na tatu kwaajili ya umaliziaji wa zahanati hiyo ili kuhakikisha inaanza kufanya kazi  na kutoa huduma kwa wananchi.

Sauti ya Bw Asheri Mkosi .

Kwa upande wake Alpha Mtuza ni Diwani wa Kata ya Chilonwa amesema ujenzi wa zahanati hiyo utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya .

Mtuza amesema kuwa zahanati hiyo itapunguza umbali kwa akina mama wajawazito wa kufuata huduma hiyo.

Sauti ya Bw. Alpha Mtuza.

Ikumbukwe kuwa Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuanisha maeneo ya kimkakati ili ujenzi wa vituo vya afya vijengwe katika maeneo hayo na kurahisisha  upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.