Dodoma FM

Jaji Mkuu aibua hoja kukabiliana na uharifu nchini

31 January 2024, 8:14 pm

Picha ni Jaji mkuu wa Tanzania prof.Ibrahim Juma leo akifungua kongamano hilo . Picha na Mariam Kasawa.

Kongamano hilo limeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kupitia chuo cha uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) .

Na Mindi Joseph.
Jaji mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma leo amefungua kongamano la siku moja la kujadili masuala ya makosa ya uharifu jijini Dodoma.

Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamisi Juma amesema uharifu unaoendelea kufanyika nchini ni pamoja na utakatishaji fedha, ufadhili wa kigaidi na matumizi ya silaha zisizo halali.

Kauli hiyo ameitoa mbele ya Majaji wa Mahakama za Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania, wananchi na wadau wengine wa sekta ya sheria walioshiriki kongamano la siku moja la kujadili masuala ya makosa ya uharifu wa kifedha jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa uhuru wa mahakama siyo kujitenga na changamoto zinazoikabili dunia, bali maafisa mahakama nchini lazima wafuate ahadi ya Tanzania ya kushughulikia uharifu wa kifedha.

Picha ni Baadhi ya Majaji na wadau wa mahakama waliokutana kwa pamoja kujadili leo hii. Picha na Mariam Kasawa.

Amesema jitihada za Tanzania zinaonekana wazi katika hatua ambayo imechukua tangu mwaka 1999, wakati ikiwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa Kundi la Kupambana na Utakatishaji Fedha Haramu wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAAMLG), lililoanzishwa mwaka 1999 jijini Arusha, Tanzania.

Washiriki katika kongamano hilo wamejadiliana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusiana na vyanzo vya athari za makosa ya uharifu wa kifedha pamoja na njia za kukabiliana na uharifu.

Kwa upande wake Dkt. Paul Kihwelo jaji wa Mahakama ya Rufani na mkuu wa chuo cha uongozi wa mahakama Lushoto anasema majaji wanatakiwa kutenda haki kwenye maamuzi ya kesi hususani katika kesi za makosa ya uharifu wa kifedha.

Kupitia kongamano hilo, mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania utatoa nafasi kushirikiana na wadau kutafuta changamoto zinazoikumba sekta ya sheria na utoaji haki.