Dodoma FM

Waandishi wametakiwa kutumia malengo endelevu kuibua changamoto za jamii.

13 May 2021, 10:39 am

Na; Yussuph Hans.

Waandishi wa Habari  wa Redio za kijamii Nchini wametakiwa kutumia malengo ya maendeleo endelevu ya  2030 katika kuibua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii zao kwa lengo la kuleta ufumbuzi.

Hayo yamesemwa na Afisa Programu wa shirika la (UNA) Goodluck William wakati akizungumza na Dodoma Fm baada ya kumalizika kwa Semina ya kuwajengea uzoefu waandishi wa Habari wa Redio za Kijamii  maswala ya maendeleo na usawa wa kijinsia yalioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali za Policy Forum, Mkoani Dar Es Salam.

William amesema kuwa ili kuboresha vipindi vya redio ni muhimu kutumia malengo ya maendeleo endelevu 2030 kwa jambo husika, ikiwa ni pamoja na malengo hayo kugusa jamii nzima kwa maslahi ya Taifa na watu wake.

Kwa upande wake Afisa Msimamizi wa masuala ya Jinsia kutoka Shirika Lisilo la kiserikali la Policy Forum Iman Hatibu amesema kuwa endapo Waandishi wa Habari watakuwa wakitoa taarifa za usawa wa kijinsia kwa wingi ndani ya jamii italeta chachu ya mabadiliko dhidi ya vitendo mbalimbali vya ukatili.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Wamelishukuru shirika la Policy Forum ambapo wamesema mafunzo hayo yamewapa ari ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya malengo ya maendeleo endelevu ili kuleta Ufumbuzi na kuwakumbusha wasimamizi pamoja Watunga Sera.

Shirika la Policy Forum limeandaa mpango mkakati wa miaka minne ambao umelenga kuleta usawa katika kugawa huduma za kijamii na utawala unaoshirikisha wananchi.