Dodoma FM

Kongwa yapongezwa kwa kupata hati safi ya ukaguzi

10 July 2023, 6:23 pm

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma mh. Rosemary Senyamule akizungumza katika baraza hilo maalum. Picha na Mkoa wa Dodoma.

Senyamule amesema kitendo hiki kimeipa heshima kubwa halmashauri ya wilaya ya Kongwa, mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla.

Na Mariam Matundu.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Kongwa kwa kupata Hati safi za Ukaguzi kwa hesabu zilizoishia tarehe 30 Juni, 2022 kwa miaka sita mfululizo tangu mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi 2021/2022.

Senyamule ameyasema hayo leo wakati wa Mkutano wa Baraza Maalumu la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2022/23.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ina jumla ya hoja 54 ambapo katika hoja hizo 39 ni za miaka ya nyuma na hoja 15 ni hoja za mwaka wa ukaguzi 2021/2022, ambapo kati ya hoja 54 hoja 16 zimeshafungwa hivyo kubakiwa na hoja 38.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa.

Kufuatia hoja 38 zilizosalia, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo kuwasilisha kwake Mkakati wa ujibuji wa hoja hizo ifikapo tarehe 30/07/2023.

Mkuu wa wialaya ya Kongwa Mh Remidius Mwema akizungumza katika baraza hilo maalum la madiwani.Picha na Mkoa wa Dodoma.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu ametoa rai kwa watumishi wote kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za utumishi wa umma ili kuepuka hoja za ukaguzi ambazo zinaweza kuepukika.

Sauti ya katibu Tawala Mkoa wa Dodoma.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema amesema Wilaya yake imekamilisha kwa wakati ujenzi wa madarasa kupitia mradi wa boost ambapo wilaya ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa Shule 2, Vyumba vya madarasa 26, madarasa ya awali 2, darasa  la elimu maalumu 1 na matundu 18 ya vyoo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kongwa.