Vijana miaka 13 hadi 35 wahanga matumizi ya dawa za kulevya
22 June 2026, 16:18

Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Juni.
Na Elizabeth Tanzania
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) imeeleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni changamoto kubwa na kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 35 ndilo huathirika zaidi.
Akizungumza na Taswira ya Habari,Afisa Mwandamizi kutoka Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya Anna Tenga amesema katika kundi hilo la vijana wengi wao wapo kwenye ngazi ya elimu ya msingi,sekondari,vyuo vya kati hadi vyuo vikuu na wasio katika mfumo rasmi wa elimu.
Amesema kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wameendaa bonanza la michezo kwa vijana mbalimbali kwa lengo la kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya.
Ameongeza kuwa ni lazima jamii kusimama na kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya kwani madhara yake ni makubwa ikiwemo kuwa na jamii ya watu wenye vitendo vya ukatili.
Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Juni ambapo kwa mkoa wa Dodoma maadhimisho hayo yatafanyika katika chuo kikuu cha St. John yakiwa na kauli mbiu “Ubunifu wa kimkakati -Suluhisho la changamoto ya dawa za kulevya” na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule.