Kairuki awaagiza TTCL Mpwpwa kuongeza kasi ya mkongo wa Taifa
23 July 2026, 17:12

Mhe. Kairuki ametoa rai hiyo Wilaya ya Mpwapwa alipokuwa akitembelea Ofisi za TTCL Wilaya hiyo na Ofisi za Posta. Amesema Dodoma nzima watu 65 tu ndio wameunganishwa. “Tunataka Watanzania wote wanufaike na uchumi wa kidigitali”
Na Stephen Noel
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angela Kairuki amewataka watumishi wa TTCL Dodoma na Mpwapwa kuongeza kasi ya kuwaunganisha Watanzania, taasisi za Serikali na za Umma katika matumizi ya Mkongo wa Taifa ili kuingia katika ulimwengu wa kidigitali.
Amesema kwa Mkoa mzima wa Dodoma ni watu sitini na watano tu waliounganishwa katika Mkongo wa Taifa na kuwataka watumishi hao kuongeza kasi ili Watanzania wote wanufaike na mkongo huo na kuwapelekea kunufaika na uchumi wa kidigitali.
Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Dodoma, Bw. Simon Marwa amesema hatua ya kwanza ilikuwa kuwaunganisha ofisi za Serikali na za Umma, hatua ya pili ni mtu mmoja mmoja na majumbani.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya hiyo wamesema kabla mawasiliano ilikuwa ni shida hasa huduma za kimtandao. Wamesema kutokana na kuboreka kwa mawasiliano katika Mji wa Mpwapwa utaimarisha uchumi na Sekta ya Elimu kwa kuzingatia Mpwapwa ni Wilaya yenye taasisi nyingi za kielimu.