Ufahamu ugonjwa wa ngozi wa Melasma na visababishi vyake
12 June 2026, 12:12

Ugonjwa huo wa Merasma hauambukizi au kusababisha kansa yoyote ila ni vema kuchukua tahadhari kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu na kujipaka mafuta ya kutosha katika kipindi cha jua kali na kutoacha ngozi kukauka.
Na Jerome John.
Jamii mkoani Dodoma imeshauriwa kujikinga na mionzi ya jua kali pindi wanapokuwa wanafanya shughuli mbali mbali za uzalishaji ili kujikinga na magojwa yatokanayo na madhara ya jua kali.
Ushauri huo umetolewa na Daktari Gregory Chono mtaalam wa ngozi kutoka Klininic ya Hallen iliyopo Makole Jijini Dodoma wakati akizungumza na Dodoma FM.
Daktari Gregory amesema kuwa kutokana na mionzi hiyo mikali ya jua mtu anaweza kupata ugonjwa wa ngozi unaoitwa Melasma na kusababisha ngozi yake ya usoni kubabuka pamoja na mashavu au maeneo ya shingoni.
Aidha Mtaalam huyo amebainisha kuwa mbali na mionzi ya jua pia ugonjwa huo unaweza kusababishwa na matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu na kupelekea mtu kubadilika maeneo hayo ya mwili kuwa tofauti tofauti.
Kwa upande mwingine Daktari huyo ameitaka jamii kuhakikisha inajikinga na mionzi hiyo ya jua wakati wa shughuli kama kilimo na hata kutembea wakati wa jua kali au katika shughuli nyinginezo.