Wataalamu waonya unywaji wa pombe kali unaweza kutengeneza taifa la wagonjwa .
15 July 2026, 17:43

Wataalamu wa Afya wameendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kujishughulisha na shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi katika unywaji wa pombe.
Na Stephan Noel.
Serikali na Asasi za Kiraia zimeshauriwa kuongeza jitihada za kutoa Elimu ya Afya kwa vijana ili kuwawezesha kujitambua na kuepuka unywaji wa pombe kali kiholela.
Rai hiyo imetolewa na Daktari Sigfrid Ishengoma alipokuwa akizungumza na taswira ya habari katika mahojiano maalumu.
Dkt. Ishengoma amesema endapo hali ya unywaji wa pombe kali kwa vijana itaendelea, siku za mbeleni nchi inaweza kupata taifa la wagonjwa wengi wa figo jambo ambalo litasababisha taifa kupata hasara kubwa na kupungua kwa nguvu kazi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wamesema migogoro ya kifamilia pamoja na msongo wa mawazo umechangia vijana wengi wa kiume na watu wazima kupenda kunywa pombe kupitiliza kwa madai ya kupunguza mawazo.
Ester Peter na Meshack Palagyo wamesema wengi wanakimbilia pombe ili kusahau matatizo lakini mwishoni wanajiletea madhara makubwa zaidi ya kiafya.