Dodoma FM

Uharibifu wa mazingira unaopelekea athari kwenye vyanzo vya maji

7 May 2026, 16:57

Shughuli za kibinadamu zinachangia mabadiliko ya tabianchi. Picha na Mtandao.

Mabadiliko ya Tabianchi ni tatizo linaloikabili dunia katika karne ya ishirini na moja na kutokana na athari zake katika nyanja mbalimbali.

Na Mariam Kasawa.
Nchi yetu imejaliwa kuwa na vyanzo vya maji vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na mito, maziwa, ardhi oevu na maji ya chini ya ardhi. Vyanzo vya maji ni rasilimali muhimu inayochangia maendeleo ya nchi, kwani tunapata maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Kutunza vyanzo vya maji ni kujiwekea mazingira mazuri ya kulinda afya ya jamii, kujenga uchumi endelevu wa nchi kwa ujumla.

Licha ya kuwepo na Sheria za Usimamizi wa vyanzo vya maji (bahari, maziwa, mito, mabwawa, na chemichemi) kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na kuwepo kwa shughuli za binadamu zinazofanyika pasipo kiuzingatia Sheria zinazosimamia mazingira na rasilimali maji.

Shughuli hizo ni pamoja na ukataji wa miti kwa ajili ya kujipatia kuni, mkaa au mahitaji ya ujenzi, mifugo, uchimbaji mchanga na madini, na ujenzi usiozingatia taratibu taratibu za mipango miji, kilimo kisicho endelevu.

Pia shughuli za uchimbaji mchanga kwenye maeneo ya mito na uchimbaji madini kwenye vyanzo vya maji, kilimo na maogesho ya mifugo katika vyanzo hivyo vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa vyanzo vya maji hususani kuongeza matope kwenye vyanzo vya maji.

Vilevile uchepushaji wa maji kutoka katika vyanzo vya maji pasipo kuzingatia sheria na taratabu zilizowekwa na serikali za uchukuaji maji kwenye vyanzo vya maji (wenye vibali vya kuchota maji kuchukua maji zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa).

Vilevile, shughuli za Kibinadamu zinachangia mabadiliko ya tabianchi (ongezeko la muda mrefu la joto la wastani la dunia) ambalo hupelekea kubadilika kwa mfumo mzima wa hali ya hewa.