Wanawake UWT watakiwa kushikamana na kuepuka migawanyiko
3 July 2026, 16:54

Wanachama wa umoja huo pia walimuomba Asia Abdallah kukubali kuwa mlezi wa umoja huo, ombi ambalo alilikubali, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi uongozi na mshikamano wa umoja huo.
Na Mwandishi wetu.
MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kutoka Mkoa wa Dodoma, Asia Abdallah, amewataka wanachama wa Umoja wa Leo Yetu Kesho Yetu kudumisha mshikamano, uaminifu na ushirikiano, huku akisisitiza kuepuka majungu, ubinafsi na migawanyiko inayoweza kudhoofisha maendeleo ya umoja huo.
Akizungumza katika uzinduzi wa umoja huo uliofanyika jijini Dodoma, Asia Abdallah, ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, amesema mafanikio ya umoja huo yanategemea zaidi mshikamano wa wanachama na utayari wa kufanya kazi kwa pamoja bila kuingiza tofauti za kisiasa, kikabila au kidini.
Amebainisha kuwa taasisi za kifedha na mabenki zina nafasi kubwa ya kusaidia vikundi vya kijamii na kiuchumi kukua, lakini akasema mafanikio hayo hayawezi kupatikana iwapo kutakuwa na migogoro ya ndani.
Amewataka wanachama kujiepusha na watu au makundi yanayoweza kuleta mpasuko kwa kutumia vigezo vya kisiasa, kikabila au kidini, akisisitiza kuwa mshikamano ni msingi muhimu wa mafanikio ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, amewahimiza kuwa na uvumilivu, nidhamu na uzalendo, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na viongozi katika kulinda amani na utulivu wa nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa umoja huo, Remigius Mubago, amesema umoja huo ulianzishwa mwaka 2024 na kuanza rasmi Agosti 27 ukiwa na wanachama 52, kwa lengo la kujenga mshikamano na kuinua hali za kiuchumi za wanachama.
Amesema hadi sasa umoja huo umeongezeka na kufikia wanachama 120, ambapo tayari wanachama 19 wamenufaika na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi zenye thamani ya shilingi milioni 27.9.
Hata hivyo, ameeleza kuwepo kwa changamoto ikiwemo baadhi ya wanachama kutofuata taratibu, wengine kujiondoa wenyewe pamoja na upungufu wa vitendea kazi vya kuendeshea shughuli za umoja huo.
Mubago amesema umoja huo unahitaji zaidi ya shilingi milioni 124 ili kutekeleza mipango yake ikiwemo kununua ardhi, kujenga ofisi, kununua basi aina ya Coaster pamoja na vifaa kama viti na matenti kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.