Wauguzi na wakunga 900 wapatiwa mafunzo elekezi
30 October 2026, 17:33

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwaimarisha wanafunzi hao katika kuunganisha nadharia waliyo jifunza darasani na uhalisia wa kazi, hatua inayolenga kuongeza ubora wa huduma za uuguzi na ukunga pamoja na kuimarisha afya ya wananchi nchini.
Na Anwary Shaban.
Takribani wanafunzi 900 wa vyuo vikuu nchini Tanzania wanaosomea shahada ya uuguzi na ukunga wamepatiwa mafunzo elekezi yatakayo waandaa kutoa huduma za afya kwa vitendo katika vituo mbalimbali vya afya nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mafunzo hayo yameandaliwa na TARAJALI (INTERNS) kwa kushirikiana na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi hao kuzingatia viwango vya ubora , maadili na weledi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na Taswira ya Habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala ya ubora wa huduma za uuguzi na ukunga kutoka Wizara ya Afya, Sir Turini Manangwa, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kutoa huduma bora na salama kwa wagonjwa wanapo kwenda katika vituo vyao vya mafunzo kwa vitendo.
Kwa upande wake, Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania , Agnes Mtawa, amesema baraza hilo lina wapatia wanafunzi hao usajili wa awali ili kuwawezesha kuanza mafunzo kwa vitendo, akibainisha kuwa vituo 40 vimeandaliwa kwa ajili ya kupokea wanafunzi hao watarajali.
Amesisitiza kuwa wanafunzi hao wanapaswa kuzingatia maadili ya taaluma , weledi na taratibu za utoaji wa huduma za afya katika kipindi chote cha mafunzo yao.
Nao baadhi ya wanafunzi hao kutoka vyuo mbalimbali vya uuguzi na ukunga wamesema wamejiandaa kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika kuwahudumia wagonjwa, huku wakiahidi kuzingatia maadili ya taaluma na kuhakikisha jamii inapata huduma bora za afya.