Dodoma FM

Wajawazito Mpalanga walazimika kusafiri kutafuta zahanati yenye wodi ya kujifungulia

26 November 2026, 16:37

Picha ni mama mjamzito anayetembe umbalimrefu kufuata huduma za uzazi . Picha na True Vision Production.

Ukosefu wa jengo maalumu la huduma za uzazi katika Zahanati ya Kijiji cha Mpalanga umetajwa kuwa changamoto inayowalazimu akina mama wajawazito kusafiri kwenda vijiji jirani kutafuta huduma za kujifungua, hali inayowaweka katika hatari ya kujifungulia njiani.

Na Victor Chigwada.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Taswira ya Habari wamesema kukosekana kwa jengo la mama na mtoto katika zahanati hiyo kunawalazimu wajawazito kujifungulia katika wodi moja na wagonjwa wengine, hali wanayoieleza kuwa haifai kwa huduma za uzazi, hivyo hulazimika kutafuta vituo vingine vyenye mazingira bora ya kujifungulia.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpalanga, Bw. Mnyukwa Sakaila, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, akisema ni kero kubwa kwa wajawazito kutokana na baadhi yao kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kujifungua, hali inayoweza kusababisha kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.

Aidha, ameiomba Serikali kujenga jengo maalumu la huduma za uzazi katika zahanati hiyo ili kuwaondolea wajawazito adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma, pamoja na kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa kujifungua, akisisitiza kuwa upatikanaji wa huduma hizo karibu na wananchi ni muhimu katika kulinda afya ya mama na mtoto.

Ripoti ya Victory Chigwada.