Dodoma FM

Wananchi waiomba serikali kuharakisha usambazaji wa maji Mlodaa

18 September 2026, 17:17

Pichani zoezi la usambazaji wa maji kwa wananchi katika maeneo mbalimbali likiendelea. Picha na DUWASA.

Wananchi hao wamesema wanategemea visima vifupi na maji yenye chumvi. Hata hivyo, uongozi wa kata umeeleza kuwa changamoto hiyo inatarajiwa kutatuliwa kupitia mradi wa usambazaji maji. Mradi huo unatarajiwa kujenga vituo 18 vya maji, malambo ya mifugo na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita laki moja za maji.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa Kijiji cha Mloda, Kata ya Mlowa Barabarani, Wilaya ya Chamwino, wameiomba Serikali kuharakisha zoezi la usambazaji wa maji ili kuwaondolea matumizi ya maji yasiyo salama kutoka visimani, pamoja na maji yenye chumvi.

Wakizungumzia changamoto hiyo, wamesema hali hiyo imewalazimu kutumia maji kutoka kwenye visima vifupi vinavyopatikana katika maeneo ya korongo, baada ya kisima kilichopo kijijini hapo kutoa maji yenye chumvi ambayo hayafai kwa matumizi.

Naye Diwani wa Kata hiyo, Anjero Lukasi, amesema changamoto ya maji katika Kijiji cha Mloda huenda ikatatuliwa ndani ya muda mfupi, kwani tayari wamepata mdau kupitia Shirika la Tanzania Light Project kwa ajili ya kusambaza miundombinu ya maji katika vitongoji vya Mloda.

Amesema kupitia mradi huo, vinatarajiwa kujengwa vituo 18 vya maji, malambo ya mifugo pamoja na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita laki moja za maji.

Simulizi na Victor Chigwada.